Je, mitandao inakutumia zaidi kuliko unavyotakiwa kuitumia?. Leo hii mtu akinunua simu kubwa (smartphone) kitu cha kwanza anachokimbilia ni kujipost mtandaoni hata kama yuko kitandani, saa ngapi hajajipost mtandaoni ili wamuone!. Je hivi ndivyo tunavyotakiwa tuitumie mitandao?
Kuwa kwenye ulimwengu wa kidigitali kunafanya watu wengi washindwe kuzikabili hisia zao, jambo lolote linalofaa machoni pake anaona ni vyema kulipost mtandaoni. Wengi hatuna uelewa hasa vijana kuhusu namna nzuri ya kuitumia mitandao ya kijamii katika miradi ya kutusaidia baadae.
Sasa wewe unajipost kila siku mtandaoni aisee, angali sana ujue u bado kijana ambaye hujui hata kesho yako itakuwaje. Picha yoyote unayopost mtandaoni hiyo imeenda, watu wataiona na itahifadhiwa kwenye algorithms milele na milele hata wajukuu zako ipo siku wataiona.
Hivyo jitahidi sana unapo-post kitu chochote kwenye social media angalau kiwe chenye maadili na inatunza heshima yako na inaleta mantiki kwa mtu yeyote. Kuna siku watu watakujaji kupitia picha hizo ulizopost huko Instagram au Twitter.
Ubaya zaidi saivi mambo yapo kidigitali zaidi kwamba mtu akitaka kukujua zaidi anakusearch mtandaoni akikutana na mambo yako ambayo siyo mazuri basi utapishana na gari la mshahara.
Chukulia mfano huu, kampuni fulani inataka ikuajiri je, ikiangalia picha zako mtandaoni utafaa kweli kupewa hiyo kazi? au watakuona kama mhuni fulani? Hii ni kwa sababu jinsi unavyojipost ndivyo unavyojielezea zaidi kuwa wewe ni nani, ni wa aina gani, unafanya nini, unapenda nini, uko makini kiasi gani?
Picha zako mtandaoni ni ushahidi tosha watu kukujua vizuri kuliko unavyojijua.
Mitandao ni sehemu ambayo unaweza kutafuta fursa za kazi, kujifunza maarifa mbali mbali kutoka kwa watu wengine. Lakini kaa ukijua mtandaoni kuna kila aina ya watu kuna watu kazi yao ni kutoa taarifa za upotoshaji, uchi na nyingine amabazo si rasmi hivyo huko mtandaoni chagua watu wa kuwafollow ili usichanganye mafaili ukaingia kwenye mtego wa panya.
Ukiona unapata taarifa ambazo siyo nzuri kwenye feed yako, fanya kuwa unfollow, kuwa block watu wote ambao maudhui yao hupendezwi nayo. Ikiwezekana zima notification za mitandao ya kijamii unayotumia kwenye simu yako ili isikuletee shida, kila dakika notification zinatokeza pale juu kwa hali hii si utakosa f ocus sasa!.
Itumie mitandao katika miradi hiyo na si kuvimbiana au kujionyesha kana kwamba upo kwenye maonyesho.
Ziko wapi ajira? Ni sauti ya kila kijana baada ya kuhitimu chuo. Mitandao ni fursa shituka, tangaza kitu kinacholeta mantiki kwa watu usitangaze hisia zako.
Saa nyingine huwa nasema hata WhatsApp kwa mwanafunzi ni sehemu nzuri ya kujitangaza kuhusu ujuzi wake you never know mtu anayeangalia status yako huenda siku moja atakuwa anafanya kazi sehemu na akakuita kufanya kazi na wewe sababu tu anajua una ufahamu wa mambo fulani. Usipost tu memes fikiria hilo pia.
Kwenye game ya kutafuta kazi mtandaoni huwa iko katika swali hili "unaweka nini kwenye akili za watu pale wanapoona ulichokipost?" Yaani mtu atafikiria nini kuhusu wewe kulingana na ulichokipost. Ifikie mahari uwe na fikra za mbali baada ya miaka mitano mbele, kile ulichokipost kitakutambulisha kama nani?
Tunaishi kwenye ulimwengu wa kidigitali ambao mtu anaweza kufanya kazi remotely, itafika muda baadhi ya ajira kama siyo zote zitakuwa zinatolewa baada ya waajiri kukuona mtandaoni unafanya kitu fulani ambacho wanauhitaji nacho.
Kutafuta kazi ni kazi. Saivi soko linakoelekea ni kwamba watu wengi watakuwa wanafanya kazi remotely, kama ambavyo freelancer wanavyotafuta kazi akishaipata na kuifanya ndo imeisha.
Na atakayepata bahati hii ni yule ambae account zake za mitandao ya kijamii inajieleza yenyewe vizuri kuhusu yeye, na yuko active. Hakutakuwa na kutuma maombi wala interview labda iwe ni lazima. Mtu huyu atashuhudia message ikiingia au akipigiwa simu zikisema
Habari,
Nimekuona kwenye mitandaoni ukielezea zaidi kuhusu blablaa ah! nimekuwa nikikufuatilia toka muda …, vipi unaweza kunisaidia kufanya hili jambo fulani?
Noah Harari Mwanahistoria alisema “We are going to believe more on algorithms than we believe in ourselves”.
Wengi bado hawaamini katika hili lakini ndo tunakoelekea miaka mitano ijayo digital platforms zitakuwa ndio kimbilio kwa makampuni, agencies na watu binafsi.
Wewe bado kijana jitahidi profile za akaunti zako ziko safi huku mtandaoni halafu kujipost siyo issue achana nayo.
Kuna kitu kinaitwa Social media profiling hutumiwa sana na wadukuzi wa taarifa mtandaoni, watu wa IT na cybersecurity wanaelewa vizuri, hii inaweza kutumika kupata taarifa zako nyeti, Vitu unavyopost Instagram, Twitter, Tiktok, vinaweza kumpa mdukuzi taarifa nyingi kuliko unavyofikiria japo wewe huwezi elewa.
Na kibaya zaidi saivi watu hawaamini udukuzi, hawaamini kabisa haya mambo ya kuhakiwa utasikia "hii technolojia bado sana kwetu, nani atani-hack mimi wakati hata pesa sina?" siku yakikutokea mimi sitakuwepo lakini nimekwambia haya mambo yapo.
Tabia ya kupost maisha yako au familia yako kwenye mitandao siyo nzuri na inaweza kukugharimu baadae.
Halafu kuna watu wanasoma cybersecurity nchi hii, subiri baada ya miaka mitano tutakuwa na vijana wengi ambao hawana ajira na kazi yao itakuwa ndiyo hiyo KUHACK maybe sharia (Cybercrime Act 2015) iwekewe mkazo.
Tumia mitandao ya kijamii katika namna ambayo haitakuja kuharibu heshima yako bali itakutangaza vyema kwenye digital world.
Kila sehemu AI, AI, AI inaenda kuchukua nafasi za wale wanaocode (Developers). Hata kipindi google inaanza watu walitabiri kuwa developers wengi watakosa kazi.
Je, developers walikosa kazi? AI ni kama google tu. Kwa nini uogope wakati maendeleo ya sayansi na technolojia yanaibua fursa zingine mpya ambapo developers wanahitajika ili kurahisisha zaidi maisha ya watu waendane na ulimwengu wa IoT?
Mfano. Mobile Application (siku hizi kila mtu anasimu), Integrated secured system (kuunganisha mifumo miwili Mfano, idara ya maji na TRA), IoT (Internt of Things), software, web based system na zingine nyingi zinazotatua changamoto mbalimbali kwenye jamii.
AI yupo anaweza kunisaidia kufanya vyote hivyo
Ndiyo, lakini kama huna ujuzi wa kucode huwezi fanya kitu chochote kwa sababu vitu vinahitaji uelewa mpana wa source code zinazotumika kutengeneza application, mifumo pamoja na kuhakikisha usalama wa data (encryption).
Hakuna AI ambayo itaweza kumwondoa developer kwenye nafasi yake, bali itamsaidia asipoteze muda mwingi katika kutengeneza programu zake.
Mtaalamu wa Ethical hacking occupytheweb aliyeandika kitabu cha Linux Basics for Hackers anasema “AI is not perfect, yet not smarter than you. It’s not going to put you out of job if you’re studying a career in tech. You need to embrace AI as tool, use it like how you use google, or else you’re going to be left behind”.
Kama ushatumia AI katika coding zako utagundua kuwa, AI inatoa data kulingana na wewe unavyotaka.
Ubora wa uulizaji wako ndio ubora wa AI kukupa taarifa sahihi vinginevyo itakupa source code tofauti na unavyohitaji, hapo utakomaa na debugging mpaka basi, hata ukiirudishia ili idebug inakuzalishia error zingine kumi.
Wale wanaosema AI inaenda kuchukua nafasi za madeveloper wengi wao hawacode, ndio wapya kwenye game (beginners), wanaoona coding ni ngumu, tena hawa ndiyo wanaopiga makelele balaa.
Wale wanaofaidi matunda ya kucode ni wale wenye title kuanzia nne yaani ni (Front-end and Back-end Developer, Network Administrator, content writer, security expert etc).
Sio lazima ujue vyote kwa ufasaha, vingine ni vizuri ukawa na basic understanding ya ni kivipi zinatumika. Usikae na kitu kimoja tu jaribu kuwa two in one (department).
Saivi kuna AI zinazotengeneza website, Apps je, madevelopers tutakaa wapi?
Je kuna AI inayotengeneza mifumo?
Iko hivi, hiyo ndiyo kazi yako jifunze pia jinsi ya kuzitumia hizo AI na ukiwa kama developer jitahidi kujua vitu kwa undani zaidi, ili hata mtu akikupa kazi uifanye kwa weledi.
Watu wengi wako shallow. Kama unajua coding na unajua kutumia AI vizuri sisi siyo wenzako tena.
Lugha. Kuwa vizuri kwenye uandishi unaoshawishi, andika content ambazo zitamfanya mtu aseme au ajisemee huyu kijana au huyu binti anajua. Iwe kwenye website, application, software au branding.
Wengi wanafeli katika eneo hili, lugha ndio itakayokutofautisha kati yako na wengine ikiwemo AI.
Kuna siku utaajiriwa au utaitwa kufanya marekesho kwenye system ya kampuni fulani, sijui utamuuliza AI? Kumbuka AI ziko limited na hauwezi kuipa source code zote za system ya kampuni hiyo ili itambue tatizo ni nini. Ni wewe na uelewa wako.
Kama utaacha kucode, ukajiunga na kundi la watu wanaosifu na kupiga makelele kwamba AI inaenda kuchukua nafasi za developers. Ni kweli hao hao developers ndio watakaochukua nafasi yako.
Hakuna muda mzuri wa kukabiliana na unemployment kama muda ambao uko chuo.
Wengi huja kulifahamu hili tayari jua limeshazama, muda huo wameshamaliza chuo wapo nyumbani, pengine hata kupata fedha ya kujikimu au ya vocha ni kipengele yaani kuipata ile buku mbili mpaka uende ukafanye kazi za vibarua ndio uipate.
Kitu kizuri ni kwamba leo hii upo chuo, unapokea boom, tukiongelea suala la bando kwako saivi siyo shida basi tumia muda huo kufanya mambo ambayo baada ya kumaliza chuo usihangaike kutafuta kazi.
Haya ndiyo mambo sita ambayo Mwanachuo Lazima Ufanye Haya ili Ukwepe Kuwa Unemployment Baadae
1. Jiunge na mitandao ya kijamii muhimu kama vile LinkedIn na Twitter
Mitandao imewatoa wengi hasa wale wasiokuwa na connection za kazi, Imewafanya wapate kazi ambazo wasingezipata kwa kutegemea vyeti vyao. Kuna watu wengi sana siku hizi wanaishi kwa nguvu ya mtandao.
Ni imani yangu kuwa tayari una account ya Twitter, Instagram, Facebook lakini nina shaka kama App ya LinkedIn unayo.
Anyways, LinkedIn na Twitter ndiko maarifa yalipo, huko utakutana na waajiri mbalimbali (Recruiters/Employers). Watu kama hawa inawezekana usiwaone kipindi unaanza ila jinsi utakavyozidi kuonyesha uwepo wako kwenye majukwaa hayo, ndivyo utakavyojiweka katika nafasi nzuri ya kuonekana kuliko wale wanafunzi wenzako.
Huko utapata kujifunza mambo kadha wa kadha yanavyoenenda kwenye tasnia yako, pia itakusaidia kuelewa mapema ni nini ufanye ili baadae usije kupishana na gari la mshahara pindi umalizapo chuo. Huko kuna watu wenye digital skills za kutosha ukiwa tu unapitia tweets au posts zao kuna mengi utajifunza.
Itakusaidia kuelewa jinsi mambo yanavyofanyika kwenye industry unayosomea. Siyo unamaliza chuo, unaambiwa nafasi zipo na zinahitaji mtu anayejua vizuri Microsoft Access ndiyo ukute na wewe ulivipuuzia kipindi upo chuo.
Katika ulimwengu tuliopo simu au laptop yako ni siraha tosha inayoweza kubadilisha historia ya maisha yako, itategemea unaitumia kwa namna gani. Jambo la kufanya install app ya Twitter au LinkedIn na ujifunze jinsi ya kutengeneza Linkedin profile nzuri sasa hivi.
2. Follow watu wanaoshare madini
Utapata maarifa mengi kwa kufollow watu wanao-share madini acha kufollow follow watu watakaokutoa kwenye reli kwa sababu mtu ukimfollow timeline yako itajaa posts zenye utopolo ndani yake.
Ubongo nao ulivyo wa ajabu utaanza kunasa na kuweka kumbu kumbu juu ya yale uliyoyaona. Medulla Oblangata itayahifadhi taarifa hizo, hatimaye na wewe unaanza kuwaza yale yale mambo yasiyo na faida kwako.
Usiingie kwenye mitandao ya kijamii kwa ajili ya kuangalia udaku na kuscroll scroll kusiko na maana bali ingia na akili ya kujifunza au akili ya kibiashara. Mitandao ipo ili uitumie ikuletee faida siyo ikutumie ikuletee hasara.
Ukikutana na post ambayo haijakupendeza. Fanya hivi:
Unfollow kama umemfollow
Mmute
Block
Hit not interested in this post
Hivi ndivyo utaweza kuchuja maudhui yapi uyaone na yapi usiyaone. Mtandaoni kuna kila aina ya watu na kila mmoja ana malengo yake usipotezwe kwenye malengo yao.
3. Tafuta Mshauri (Mentor)
Ukiwa chuo kuna mambo mengine huwezi kufundishwa au utafundishwa ila ukija mtaani function yake ni sifuri kwa hiyo ni vizuri ktafuta mtu ambaye tayari yupo kazini au anakifanya hicho kitu unachotamani baada ya kumaliza chuo uwe unakifanya na wewe.
Mfano kama unasoma Business management hakikisha unakuwa na mtu ambaye yupo kwenye industry, kupitia kwake atakufundisha mambo mengi, atakupa guidance ya wapi ukazie, soko likoje, unatakiwa ufanye nini kwa sasa n.k
Mentor siyo lazima awe mtu ambaye unaonana naye uso kwa uso. Unaeweza kumpata mentor kupitia mitandao ya kijamii so huyo ndio utakuwa unamfuatilia kila hatu kwenye social media zake au kupitia kusoma vitabu vyake kama ameandika ila ukipata wa kuonana naye itakuwa vizuri zaidi.
4. Ongeza maarifa kupitia Online Courses
Internet imerahisisha maisha, leo hii unaweza kusoma popote ulipo na cheti ukitaka unapewa. Ulimwengu tulio nao bila kunoa ujuzi wako utajikuta unapitwa na wakati kila siku.
Jifunze maarifa mapya kila siku, watu wanaoweza kujitofautisha na kupata fursa kidigitali ni wale waliowekeza nguvu zako katika kujifunza maarifa mapya ama kujiendeleza katika career zao. Huwezi kuwa vizuri ikiwa huna utaratibu wa kunoa ujuzi wako kila siku.
Vijana wengi chuoni hawanaga muda kabisa wa kuchukua course mtandaoni kujifunza maarifa mbali mbali basi wewe jitahidi kuwa mtu wa tofauti chukua hizo courses nakwambiaje lazima tu utawazidi kwa kiasi chake halafu zisake fursa zinazoendana na maarifa uliyoyasoma.
Course yoyote unayoitaka inapatikana mtandaoni ni suala la kuchukua simu na kuingia YouTube, andika course unayotaka usome mfano, Project Management full course, kwa click moja unamaliza course ukiwa na maarifa ya kutosha.
Pia kuna majukwaa mengi ambayo unaweza kuchukua course unayoitaka kama vile Linkedin learning, Udemy, Coursera, HubSpot, Class Central n.k huku unafundishwa real life experience tofauti na mwalimu darasani anaekufundisha ili amalize syllabus.
5. Anza kufanya kazi ukiwa bado upo chuo (freelancing au virtual internship)
Tafuta kazi ambazo unaweza kufanya ingali bado unasoma, ukiwa chuo ndio muda wa kujitolea kwenye taasisi, kampuni mbalimbali. Fanya kazi as a freelancer kwenye majukwaa mbalimbali kama vile Upwork, Fiverr, ukiwa mtandaoni unaweza pia ukawa unapata kazi za hapa na pale.
Muda mwingine vitu unavyofundishwa darasani nitofauti kabisa na vile vinavyofanyika kwenye industry, hivyo ni bora kuyajua haya mapema na kuyafanyia kazi ili pindi utakapomaliza chuo isiwe changamoto kwako.
Usisubiri mpaka umalize chuo ndio uanze kuomba kazi. Anza sasa hivi najua unajua kule nyumbani hali ilivyo yaani kupata kazi ni mtiti, ukimaliza chuo ukaenda nyumbani, ndiyo imeisha hiyo.
6. Kuwa vizuri kwenye lugha (written and spoken)
Asilimia 90% ya mazungumzo mtandaoni hufanyika kwa njia ya maandishi, hivyo ni vizuri ukajinoa zaidi katika kuandika na kuwasilisha maudhui/ujuzi wako kwa watu.
Njia nzuri ya kujinoa ni kuanza leo kwa kuandika mawazo uliyonayo kichwani kwenye notebook au applikesheni yoyote ikiwezekana uwe unapost huko mtandaoni hata kama kiingereza au kiswahili kimekaa upande. Post leo, kosea jifunze tena mdogo mdogo mwisho wa siku unakuwa vizuri.
Ukiwa chuoni jitahidi kupost kila siku au mara mbili kwa wiki ikiwa vipindi vimebanana sana. Ule muda unamaliza chuo, utakuwa na kundi kubwa la watu wanaokuhitaji ufanye nao kazi au uwafanyie baadhi ya kazi zao.
Mitandao huwa haina maana saana kwa macho ya mwanafunzi lakini subiri umalize ndio utajua umuhimu wake. Haijalishi unasomea nini kuwa na digital presence ni lazima, unaona akina Mo Dewj wako kule unafikiri masihara!
Muhimu: Post vitu vya msingi ambavyo mtu akisoma aseme kweli huyu kijana au huyu dada anajua.
7. Kuwa mtu mwenye haiba (personality) ili umma wa digitali uvutiwe na wewe
Kila siku jitahidi kuwa mtu wa tofauti na wengine, fanya vitu ambavyo watu wengi hawavifanyi ilimradi unaviamini, ni halali.
Kuwa mtu wa kujifunza kila kukicha kwa kusoma vitabu, articles, hudhuria mikutano, seminar au online events.
Tatizo la ajira halitakaa liishe bali litaongezeka maradufu. Juhudi zako tu ndizo zitakazokuokoa.
Hakuna chuo kinachoweza kukufanya ukwepe kuwa jobless baadae, zaidi ya kuweka juhudi zako binafsi katika kuitengeneza kesho yako. Hatima ya maisha yako ipo mikononi mwako.
Sikuwahi kuamini kama Linkedin ingeweza kunisaidia kupata mteja kwani wanafunzi wengi tunaamini mtandao pekee hauwezi kukufanya upate kazi zenye maana mpaka uajiliwe kwenye makampuni au taasisi.
Jambo ambalo linatufanya tuwe na mawazo mgando na hatimae tukose fursa zilizo ndani ya uwezo wetu.
Ilikuwaje mpaka nikapata mteja?
Kitu kilichonisadia hadi nikapata mteja ni kupitia posting zangu ambazo nilikuwa nikipost kila mara huko linkedin kulingana na tasnia yangu.
Hali yangu ya kupost mara kwa mara ndiyo iliyojenga uaminifu, kutosahaulika na kuonekana kuwa mtu ambaye ninaweza kufanya kitu fulani.
Hivyo, siku moja nimejichokea zangu ghafula napigiwa simu, “Hello! wewe ndiye Anthony? Yes (nilijibu), nimekuona linkedin unazungumzia mambo ya ………. Na nimeangalia kwenye profile yako umejitambulisha kama web developer, hivyo unaweza kunitengenezea website? ….”
Kuanzia hiyo siku nikaamini mambo yanawezekana endapo tu utaweka juhudi, uvumilivu na nguvu katika kile unachokipambania. Linkedin ni mtandao unaoweza kumfanya mwanafunzi apate fursa za kazi as a freelancer hata kama bado anasoma.
Ninawezaje kushiriki katika jumuiya ya Linkedin hali ya kwamba mimi ni Mwanafunzi?
Kama ninaweza kuwa online masaa mawili Instagram au facebook nikiscroll up and down, nashindwaje kuutumia muda huo kuandaa maudhui au kushiriki na wenzangu katika jukwaa la Linkedin? Ule mda ambao wewe uko Tiktok, Facebook, mimi ndo naandaa maudhui halafu baadae naingia kwenye kipindi kama kawaida.
Naweza kusema kwamba kama wewe ni mwanafunzi basi unaweza kujisogeza taratibu kwenye jukwaa hili la Linkedin, mtandao ambao unakufungulia dunia kuwa unachotaka.
Bila shaka unatamani kujua website niliyomtengeneza mteja, haikiuchukua muda website ikakamilika nayo ni Better Careers. Tofauti na hilo kuna watu wengi pia walionitafuta inbox hivyo kutokana na uzoefu wangu mchanga baadhi ya fursa nilichengana nazo.
Tofauti na hayo jukwaa hili limenisaidia kujifunza mambo kadha wa kadha kwa kusoma post za watu wengine, kuangalia mabadiliko ya teknolojia yanavyokwenda mbio (AI), kupitia Linkedin learning huwezi amini linkedin ndiyo mtandao ambao mimi nilianzia kusoma Web Development kipindi hicho hata opening tag <> or </> sizijui.
Linkedin ni mtandao wa watu wenye vyeo vyao, watu wanaojua kingereza vizuri
Kipindi najiunga linkedin sikuwa naelewa wapi nianzie na wapi niishie kwa sababu ukiangalia kila mmoja kwenye post zake alikuwa anatema ng’eng’e hatari. Nikawa najisemea kimoyo moyo aisee huu utakuwa ni mtandao wa watu fulani fulani hivi wenye vyeo vyao.
Kwa kuwa mwanzo huwa ni mgumu nikiwa kule nilikuwa kama mtazamaji, mzee wa kuscroll down and up yaani nikitaka kuandika post, hizo ng’eng’e kuzipangilia ilikuwa ni issue.
Mdogo mdogo we mwendo, ayeeya mwendo nikaanza kuandika na kusoma vitabu, unaambiwa mazoea hujenga tabia, ee bwana tabia yangu ya kuandika ilianza kukua taratibu na ndipo upweke wa kusema linkedin ni mtandao wa watu wenye vyeo vyao ukanitoka.
Unajua kule LinkedIn watu wengi wanatumia kingereza kwa sababu watumiaji wengi wa Linkedin hawajui Kiswahili lakini sasa hivi unaweza kutambaa na Kiswahili kuiteka hadhira unayoilenga.
Njia pekee itakayokusaidia wewe usiteseka na barua za internship wala usisumbuke na ajira baada ya kumaliza chuo ni Linkedin inaweza kuwa miongoni mwake.
Naitwa Anthony Charles natengenza tovuti mbalimbali | Mwandishi, pia nasaidia wanafunzi wenzangu walioko chuo kuhusu namna mbalimbali za kukabiliana na unemployment.
Linkedin ni mtandao wa kidigitali ambao unaunganisha watu wa kila aina kutoka pande zote za dunia hasa vijana wanaotafuta kazi, wajasiriamali wanaotaka kukuza biashara zao, kuboresha kazi zao na makampuni yanayotafuta wafanyakazi nayo pia yapo Linkedin.
Unaweza kuchukulia masihara ila wataalamu wengi wako kule yakiwemo makampuni, kule watu waliotengeneza jina wanaingiza pesa bila hata kwenda ofisini kuomba kazi, wengi wanafanya kazi kama freelancer.
Jinsi ya kujiunga linkedin
Kuna namna mbili za kujiunga linkedin, namna ya kwanza ni kusanikisha/kuinstall linkedin app kupitia Play Store au App Store. Andika Linkedin app kwenye search bar bonyeza iyo application ya blue kisha install. Baada ya kuinstall endelea na usajili, Linkedin app itaonekana kama hapo chini.
Namna nyingine ni kujisajili kupitia website ya LinkedIn.
Anza usajili wako kwa kubonyeza hii link LinkedIn Signup, jaza taaarifa zinazohitajika (Email,Password). Hakikisha unaweka kumbukumbu juu ya taarifa unazoziweka ili kuondoa usumbufu unaoweza kujitokeza baadae kama utasahau neon siri.
Mara nyingi watu wamekuwa wakisahau email na password walizotumia kujiunga LinkedIn, bahati mbaya hakuweka two factor authentication hivyo akisahau password au email uwezekano wa kuirejesha akaunti yake unakuwa mgumu sana.
Wengi wamekuwa wakitelekeza akaunti zao hivi hivi, unakuta alikuwa ameanza kupata followers engagement, ameanza kutambulika.
Narudia hakikisha email na password unaikumbuka vizuri.
Baada kujiunga, watakutumia ujumbe kwenye email yako ili kuthibitisha kama gmail yako iko active, kinachofuata ni kumalizia usajili kwa kujaza taarifa zako ipasavyo kwani hizo taarifa ndizo zitakazokaa kwenye profile yako ya LinkedIn
Hii hatua kitaalamu inaitwa profile optimization.
Tayari Tumeshatengeneza Akaunti, Sasa Twende Tukaifanye Profile Yako Iwe ya Kitaalamu (Profile Optimization).
Awali ya yote Linkedin siyo facebook, huku kidogo inabidi ujiweke katika mazingira mazuri uonekana as a professional huku ndiko wateja wako walipo na ndiko utakapopata fursa mbalimbali za kukutana na watu, kushare idea, kubadilishana mawazo na watu mbalimbali kulingana na tasnia uliyopo.
Bila kupoteza wakati haya ni mambo muhimu inabidi uyafanye ili kuboresha profile yako.
1. Profile picture.
Hakikisha picha unayoweka kwenye profile inakutambulisha kama mtaalamu kwenye tasnia yako. siyo unapiga selfie ndio unatuwekea kwenye profile, Recruiters, wateja watakuona hauko serious. Picha hiyo iwe karibu na kamera, ionekane vizuri. Picha yako ndiyo utambulisho wako.
2. Banner.
Hapa utaweka background picture, texts au quote inayoendana na fani yako. Size ya background image huwa ni 1128 x 191. Wengine pia huweka namba zao za simu na email. Ni vizuri ukachagua kipi kinafaa uweke kuliko kuacha blank. Angalia mfano hapa chini.
3. Kichwa cha profile yako.
Hapa nazungumzia jina lako kamili na headline title ambayo itaonekana mwanzoni kabisa mwa profile yako. Hakikisha headline inajibu wewe ni nani, unasaidia nini?
Kufanikisha hili angalia hapo juu kushoto kuna kitufe kama kalamu bonyeza hicho na jaza taarifa zinazohitajika. Mfano Headline* yangu ni Built my brand while in college from 500+ to 7k people. Helping you do the same. Web developer & designer | Content Writer.
4. Kazi na Elimu.
Ili kuifanya profile yako inawili vizuri, hapo hapo kwenye profile kuna sehemu imeandikwa Open to work bonyeza hicho kipenseli, halafu weka cheo cha kazi unayofanya (job title) n.k
Ukishafika kwenye visibility ruhusu recruiters only, hiyo nyingine siyo nzuri kuitumia kama kweli wewe unataka uonekane mtaalamu katika tasnia yako.
5. Experience/uzoefu
Pia utashuka chini kwenye Experience, hapo utaweka shule, makampuni au taasisi ambazo umeshawahi kufanyanayo kazi. Elezea kwa kiasi gani umeshiriki katika kuongeza ujuzi wako, vitu gani ulifanya n.k.
6. About
Hapa inatakiwa uelezee fani yako japo kwa kifupi, weka bayana nafasi uliyopo kwa sasa, unafanya nini, unatatua changamoto zipi, kwa namna gani, uzoefu wako ni upi kisha unaweka vitu ambavyo unaweza kuwasaidia watu wengine. Angalau ianzie aya mbili.
7. Mpangilio/Setting.
Mkono wa kulia juu kwenye profile yako kuna ikoni ya setting, ibonyeze shuka chini kidogoshowing profile photo ruhusu kwa linkedin members wote.
8. Usisahau kuwasha creator mode.
Hapa utaweka vitu utakavyokuwa unaongelea katika machapisho yako ya kila siku. Kwa kufanya hivi naamini kwa asilimia 90 profile yako itaonekana bora na ya kiprofessional zaidi.
Tumalizie, Linkedin pia inatoa fursa ya kujifunza course mbalimbali bure ndani ya mwezi mmoja. Je unapataje ofa hii?
Ni rahisi tu, pale unapoingia linkedin home page kwa juu mkono wa kushoto kunaonekana profile picture yako, ibonyeze halafu angalia chini wameandika activate premium, pabonyeze halafu endelea na maelekezo.
Baada ya hapo unaweza kujiunga linkedin learning ukapiga course mbali mbali ukishamaliza unapewa na cheti kabisa, ni wewe tu kufanya maamuzi leo.
Muhimu: Kuwa makini kwenye Akaunti utakayotumia kwenye premium kama unaona siyo vizuri kutumia kadi yako ya bank unaweza kutengeneza M-Pesa VISA Card bure ndani ya dakika moja.
Baada ya kufanya hivyo inabaki kazi ya kujimwanga kwenye jukwaa kuwakilisha kile ulicho nacho hapa naongelea kupost, kushiriki kwenye mazungumzo na jumuiya ya Linkedin, kuendelea kuwa hai.
Baada ya Yombo kusikia neno AI linatamkwa sana huku mtaani ikabidi amuulize jamaa yake Kadozo ili apate kujua zaidi.
Hivi ndivyo Mazungumzo yalivyokuwa.
(Kadozo na Yombo ni vijana wanaosoma chuo, BBM)
Yombo: Je, unafahamu chochote kuhusu teknolojia ya AI?
Kadozo: Ndiyo, na nimekuwa nikisoma vizuri kuhusu maendeleo ya kuvutia yanayoletwa na AI, kama ulishawahi kusoma the discovery of fire basi hii ni discovery of AI.
Labda kabla hatujaendelea nikuulize, hivi unajua kwamba AI sasa inaweza kutumia sauti yako kuanzisha mazungumzo na mtu mwingine?
Yombo: Hapana? Mbona hii ni ya kushangaza! Inakuwaje na Inafanyaje kazi?
Kadozo: Vizuri, mifumo ya AI inaweza kuchambua, kuiga sauti ya binadamu au rekodi za sauti ili kuunda mfano wa sauti itayotumika na AI.
Mfano, sauti hii ninayoitoa kama itarekodiwa, AI inaweza kukopi na kutumia sauti hii hii kuzalisha maneno yaliyosanifishwa ambayo katika kuongewa kwake yatafanana sana na sauti yangu.
Yombo: Oooh! Very interesting, Lakini inaanzishaje mazungumzo na mtu mwingine?
Kadozo: Mara tu AI inapokuwa imesanifisha sauti, inaweza kutumia algorithms za usindikaji wa lugha asili kuchambua na kuelewa maudhui ya mazungumzo yenu kisha kuzalisha majibu yanayofaa na kushiriki katika mazungumzo na mtu mwingine. Yaani kama AI itaanza kwa kusema hello! na wewe ukajibu-
Hapo ndipo mazungumzo yanapoanzia kwa sababu itakuwa inajibu na kuuliza maswali kulingana na majibu yako. Kumbuka hapa itatumika tu kama imetengenezwa kwa lengo la kuongea na mtu mwingine.
Cha kuongezea tu ni kwamba ni kivipi sauti yako inaweza kuchukuliwa na AI?
Moja kati ya njia ni kutumia kumbukumbu za sauti yako iliyonakiliwa awali, kama vile sauti zilizorekodiwa za mahojiano au hotubaKisha, AI inatumia teknolojia ya kujifunza ili kujenga mfano wa sauti yako na kuitumia.
Moja ya njia zinazotumika kurekodi sauti yako ni voice cloning . Njia nyingine ni kutumia sauti yako inayopatikana kwenye mitandao ya kijamii.
Kadozo: Kwa hivyo, AI inaweza kimsingi kutumia sauti ya mtu na kuwa na mazungumzo yenye maana na watu wengine?
Kadozo: Ndio, hilo halina ubishi. Unaambiwa huwezi kumnasa samaki aliyefumba mdomo kwa kutumia ndoano.
Kwa hiyo AI inaweza kusikiliza kile mtu anasema, kuiga habari hiyo na kujibu kwa njia ambayo inasimulika kama mazungumzo yanayofanana na ya binadamu.
Yombo: Duh! hii mpya, Jambo usilolijua ni kama usiku wa giza. Napata kujiuliza maswali mengi sana ya usalama?
Kadozo: Maswali gani hayo tena Mr. Yombo?
Yombo: Sasa kama ni hivyo mfano si AI inaweza kutumiwa ili kupata taarifa zangu binafsi za shule kama itaiga sauti ya registration officer?
Kadozo: Bila shaka. Matumizi ya AI kufananisha sauti ya mtu yanazua wasiwasi kuhusu faragha, wizi wa utambulisho, na matumizi mabaya ya habari binafsi.
Lakini nikwambie kwamba katika ulimwengu tuliopo usimwamini mtu yeyote anayehitaji taarifa zako, pia tumia “multifactor authentication” ili kama humwelewi umwambie atumie njia ya pili kuwasiliana na wewe.
Kwa kawaida AI ukiiuliza wewe ni ni nani itasema Mimi ni kompyuta program niliyeundwa blablaa.
Hapa chini tulipata kumuuliza ChatGPT na alitoa majibu yafuatayo.
Sasa karibia kila aina ya AI huweza kujitabulisha kulingana na ilivyopangiliwa. Hapa ni rahisi sana kujua kumbe unaongea na AI.
Mfano, Assume ChatGPT ingebatizwa kwa jina lako la Yombo, hapo juu ingesema “Mimi ni Yombo blablaa” chukulia ndiyo unaongea nayo kwenye simu, hapo si ni rahisi kuamini unaye ongea nae ndiye bwana Yombo? Hivyo ndivyo mambo yanavyoenenda ndugu yangu.
Tunaishi katika wakati ambapo teknolojia inabadilika kwa kasi, na AI inachukua jukumu kubwa katika mapinduzi hayo. Lazima tuwe wazi na tayari kukabiliana na changamoto na masuala mengine yanayoweza kujitokeza.
Yombo: Hiyo ni uhakika. Nashukuru sana ndugu yangu kwa kunitoa gizani, siku nyingine nitakutafuta tuangazie mambo mengine kwa undani zaidi.
Kadozo: Haina noma mshikaji wangu.
Unaweza ukawa unajua kuwa watu wote wanajua kumbe hawajui. Kama una swali lolote dondosha coment yako hapo chini utajibiwa.